Nairobi, Kenya, January 22- Msanii maarufu na mwenye uzoefu wa muda mrefu, Yusuf Kombo, anayejulikana kwa jina la kisanii Susumila, atakuwa miongoni mwa wasanii wa kwanza barani Afrika kuwa na tamasha kubwa mwezi Januari.
Susumila atatumbuiza katika tamasha la Burudani Experience, ambalo linakuwa msanii wa pili kufuatia kuanzishwa kwa mfululizo huu wa matamasha yanayofanyika kila mwezi. Onyesho hilo litaandaliwa katika ukumbi wa Alliance Française, Mombasa, Ijumaa, tarehe 24 Januari, kuanzia saa kumi na moja jioni. Susumila ataungana na Pinto The Band kutoa burudani ya hali ya juu.
Hii ni nafasi ya kipekee kwa wanamuziki, wapiga vyombo, mashabiki, wanahabari, na wadau wote wa sanaa kukutana, kufurahia muziki wa moja kwa moja, na kuwaunga mkono wasanii wa ndani. Kulingana na waandaaji wa tamasha, kiingilio kitakuwa bure, hivyo kila mtu anaalikwa kuhudhuria.
Historia ya Tamasha na Mipango ya Kaa la Moto
Kaa la Moto, mwanzilishi wa tamasha hili, alianza mfululizo wa Burudani Experience mwaka jana akishirikiana na msanii Echo254, ambapo tamasha la kwanza lilifanikiwa. Kupitia mitandao ya kijamii, Kaa amehakikishia mashabiki na wasanii kwamba kila mmoja atapata nafasi ya kutumbuiza mwaka huu. Kwa kuanza, amemchagua Susumila kufungua mwaka huu wa 2025.
Kupitia mtandao wake wa Facebook, Kaa aliandika:
“2025 ni mwendo wa solutions tu kwa sanaa yetu. Hakuna muda wa lawama au kuongelea matatizo! BURUDANI EXPERIENCE sio tu show, ni mahali pa kuonana, kubadilishana mawazo, na kupata burudani ya moja kwa moja bila playback. Wasanii wote mjitokeze, kila mmoja atapata zamu yake. Kiingilio ni bure pale Alliance Française, Mombasa. Mashabiki, tujaze ukumbi na tuunge mkono muziki wetu wa ndani. Tunaanza na Susumila Yusuf. Let’s celebrate our own music and artists. See you from 5 PM!”
Mafanikio ya Susumila katika Live Performances
Ikumbukwe kuwa Susumila si mgeni katika masuala ya live performance. Tayari ameshafanya matamasha kadhaa, likiwemo lile la hivi karibuni katika mgahawa wa New Cheers, Nyali, ambapo alitoa burudani ya kipekee.
Miongoni mwa nyimbo zinazotarajiwa kutumbuizwa ni pamoja na Sianzi Leo, Sonona, Ngoma Itambae, na vibao vingine vinavyopendwa na mashabiki.
Susumila ni msanii mwenye rekodi nzuri, akijulikana kwa kazi zake za ndani ya studio na hata za nje. Mashabiki wake wamekuwa wakimsifia kwa juhudi zake, hasa baada ya tamasha la kufunga mwaka katika Buntwani, ambalo lilimletea mafanikio makubwa, ikiwemo kununua simu mbili za iPhone.
Kwa hakika, onyesho hili la Burudani Experience linatarajiwa kuwa mwanzo mzuri kwa mwaka 2025 katika tasnia ya muziki wa moja kwa moja. Usikose!