Mombasa, Februari 6- Mwezi uliopita ulijaa matukio mengi, hasa kwenye sekta ya sanaa na muziki hapa nchini. Moja ya masuala yaliyogonga vichwa vya habari ni sakata la baba na mwanawe kuhusu muziki, lililozungumziwa sana katika Ukanda wa Pwani.
Shephard Washemakinz, msanii wa muda mrefu kutoka Pwani, alionekana kumrithisha kipaji chake msichana wake Mishy, ambaye pia ni msanii. Hata hivyo, wawili hao walikuwa katika mvutano juma lililopita, ambapo baba alionekana kumkataa mwanawe kujiingiza kwenye muziki.
Katika mahojiano na The Rush Hour kupitia simu siku ya Jumatatu, Shephard alielezea kuwa sanaa, hasa muziki, una changamoto nyingi kwa wasichana, ikiwa ni pamoja na dhuluma za kijinsia. Alisema kwamba asingependa mtoto wake aingie kwenye tasnia hiyo kutokana na changamoto hizo.
Hata hivyo, baada ya mahojiano hayo, Shephard alipokea ushauri kutoka kwa watu wa karibu na kibiashara, ambao walimsaidia kuona athari za kumkatalia mtoto wake kuendeleza kipaji chake. Hivyo, alibadilisha mtazamo wake na kuingia studio na Mishy kuachilia kazi mpya pamoja.
Shephard ameshirikishwa katika wimbo mpya uitwao “Sawa”, ambao umeanza kufanya vizuri mtandaoni, hasa kwenye YouTube. Wimbo huo uliachiwa rasmi siku tatu zilizopita, na video yake imetengenezwa na Mrima, huku audio ikitayarishwa na Multi Million Empire na Master Bram. Wimbo huo unatarajiwa kuwa moja ya kazi kubwa za msichana huyo.
Ni muhimu kutambua kwamba Mishy alikuwa akiachilia muziki hata kabla ya sakata la kumkatalia na babake. Katika ngoma yao mpya, ambayo inazungumzia masuala ya Mishy kulalamika kutosaidiwa na babake katika kukuza kipaji chake, huku babake akimjibu kuwa sanaa ina changamoto nyingi kwa watoto wa kike, wimbo huo una maudhui yanayogusa maisha ya wasichana wengi wanaokutana na changamoto kama hiyo.
Shephard na Mishy wamejiunga na orodha ya wasanii na familia zinazojivunia kuwa na wazazi ambao ni wasanii pamoja na watoto wao. Miongoni mwa familia maarufu ni Fat s na mwanawe Hajj Mahela, Daddy Q na mtoto wake Marsh Mashav, kule Bongo kuna Zuchu na mama yake Khadija Kopa, ambao wote wanafanya vyema.
Je, unaweza kumkataza mtoto wako asifanye kazi unayoipenda? Na je, itakuwa sawa ikiwa yeye mwenyewe anapenda?