Mombasa, Agosti 14- Kundi maarufu linalokua kwa kasi zaidi mkoani Pwani, Wakanda254, limeendelea kujizolea umaarufu na kuzungumziwa kila kona. Kundi hili lilianzishwa miaka miwili iliyopita na Boss Ivan, raia wa Uganda anayeishi Kenya na mfanyabiashara anayependa sanaa.

Upendo wake kwa filamu Wakanda Forever ulimchochea kulitaja kundi kwa jina hilo, ingawa yeye mwenyewe si msanii, bali mlezi wa vipaji chipukizi.

Tofauti na makundi mengi ya muziki, Wakanda254 wote wako chini ya mwavuli wa biashara ya Boss Ivan. Wasanii hao, ambao pia ni wafanyabiashara, wameonesha umoja na nidhamu kubwa, wakijivunia safari zao zilizopitia changamoto mbalimbali. Kundi lina wanachama zaidi ya 20, ingawa idadi hubadilika kulingana na mtindo wa nyimbo.

Baadhi yao ni Kasso Kenya, Osman Tyno, Kibo The Beast, Dhudhu X, Leno Ke, Bisti Kibo na Petit Movadi ambaye huimba Kilingala, jambo linalowafanya wengi kudhani anatoka DRC Congo.

Wameachia nyimbo kama Mama, Mukome, Boss Kama Boss, Dear Ex, Yeye Tu na Cheza. Kwa sasa wanatamba na kolabo yao na K.O Kenya, huku wakitarajiwa kushirikiana na Dogo Richie na Echo254. Hii inafuatia kolabo yao ya kwanza kabisa na Jimbi.

Licha ya kuwa na mwaka mmoja tu kwenye tasnia, Wakanda254 wamekuwa gumzo mitandaoni, wakijibizana na majina makubwa kama Kelechi Africana na kuongelewa na wasanii wengine akiwemo Tee Hits na Vincent Kras. Mapema mwezi huu, waliandaa tamasha lao la kwanza, The Night of Wakanda, katika ukumbi wa Donbay, Rabai, na kujaza nafasi zote.

Katika mahojiano na Mo Radio mwezi uliopita, Wakanda walisisitiza kuwa hakuna sababu yoyote inayoweza kusababisha kundi kuvunjika, wakijitofautisha na makundi yaliyosambaratika kama Sauti Sol, Yamoto Band na mengine.

Kwa sasa, Wakanda254 ndio wasanii wanaotajwa zaidi Pwani, swali ni, je wataendelea kutamba na kufanikisha ndoto yao ya kuteka jiji na kuingia kwenye ramani ya muziki kitaifa?

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *