Mombasa Julai 28- Kocha wa timu ya soka ya Shule ya Upili ya Serani, Alex Shikanga, amewahakikishia wapenzi wa soka kutoka ukanda wa Pwani kuwa kikosi chake kipo tayari kuiwakilisha vyema eneo hilo katika mashindano ya kitaifa ya shule za upili, yanayotarajiwa kuanza kesho, Julai 29 hadi Agosti 2, 2025, katika Kaunti ya Kakamega.
Serani, mabingwa wa ukanda wa Pwani, wamepangwa katika Kundi A pamoja na shule zenye ushindani mkali kama Highway kutoka Nairobi, Kirangari ya eneo la Kati, na St. Joseph’s Boys ya Kitale. Hata hivyo, Kocha Shikanga amesema ana imani vijana wake wataonesha ubabe wao kwa kuandikisha matokeo bora zaidi mwaka huu, kutokana na maandalizi ya kina ambayo wamepatiwa.
Akizungumza na meza yetu ya michezo kabla ya kuondoka kuelekea Kakamega, Shikanga alieleza masikitiko yake kuhusu ukosefu wa msaada kutoka kwa viongozi wa Kaunti ya Mombasa. Alisema ni jambo la kusikitisha kuona viongozi wa ngazi za juu, akiwemo Mbunge wa Mvita na Gavana wa Mombasa, wakikosa kuiunga mkono timu hiyo licha ya kuwa inaiwakilisha kaunti hiyo kitaifa.
“Hawa ni vijana wenye nidhamu, bidii na kujituma, lakini hawatambuliwi wala kupewa motisha. Inavunja moyo kuona kuwa hata baada ya kuibuka mabingwa wa ukanda wa Pwani, hakuna kiongozi aliyejitokeza kuwapongeza au kuwasaidia kwa njia yoyote,” alisema Shikanga.
Hata hivyo, aliwatia moyo wachezaji wake kutokata tamaa, na badala yake kutumia hali hiyo kama motisha ya kuonyesha ubora wao uwanjani. “Tutaingia uwanjani tukijua kuwa tunawakilisha Pwani nzima, na lengo letu ni kufika mbali zaidi—na hata kutwaa taji,” aliongeza.
Ripoti imeandaliwa na Omar Mazera – mwanahabari wa Mo Radio.