Mombasa, Julai 30- Baada ya kushindwa kusalia katika Ligi ya Kitaifa ya NSL na kushushwa hadi Ligi ya Daraja la Kwanza, klabu ya SS Assad kutoka Ukunda, Kaunti ya Kwale, sasa imechukua hatua ya mabadiliko kwa kumteua kocha mchanga Daniel Lenjo kuiongoza kwa msimu ujao.
Kocha Lenjo, awali alikuwa naibu kocha wa klabu ya bandari, kocha mkuu wa bandari youth, kocha wa shule ya upili ya serani pamoja na kusimamia akademia ya soka ya Club Fit For Life mjini Mombasa, amesema uteuzi wake ni heshima kubwa na ameahidi kujitolea kikamilifu kuifanyia klabu hiyo mageuzi muhimu.
Akizungumza na meza yetu ya michezo, Lenjo alieleza kuwa tayari ameanza maandalizi ya msimu ujao huku akidokeza kuwa wachezaji wengi wa kikosi kilichoshiriki msimu uliopita wameachiliwa huru, na kubakiza wachezaji sita pekee.
SS Assad, ambayo ni moja wapo ya klabu tajika kwa kulea vipaji vya hali ya juu ikiwemo mshambulizi wa Bandari FC na timu ya taifa ya Harambee Stars, Beja Nyamawi, imekuwa ikikumbwa na matatizo ya kifedha na changamoto za kiutawala ambazo zinatajwa kuchangia kuporomoka kwake.
Kocha Lenjo amesema anasaka wachezaji wapya vijana, wenye vipaji na gharama nafuu ili kuhakikisha klabu inarejea kwenye hadhi yake bila ya kuathirika kifedha. “Tutalenga wachezaji ambao si tu wenye uwezo wa juu uwanjani, bali pia wale wanaoweza kuhimili changamoto za kifedha za klabu,” alisema.
Lenjo aidha amesema lengo lake kuu ni kuiwezesha SS Assad kurejea katika Ligi ya NSL, na hatimaye kuijenga klabu hiyo kuwa na msingi imara wa maendeleo endelevu ya soka ukanda wa pwani.