Mombasa, Kenya, October 14 – Mwanahabari maarufu ukanda wa pwani Robert Matano ambaye anajulikana kama Robby Dallaz ameweza kufunguka kuhusu maisha na safari yake hadi alipofikia.
Robby ambaye ni miongoni mwa watangazaji wenye vipaji vingi kuanzia usanii, upigaji picha na video na kazi nyenginezo, ameelezea ugumu wa maisha na alipotoka.
Kupitia The Hotseat live ya Mo radio siku ya Ijumaa 11 Oktoba 2024, Dallaz amesema kwamba baada ya kumaliza shule ya upili akajitosa kwenye kazi ya boda boda angalau kujipatia kipato baada ya kukosa karo ya kuendeleza masomo yake.
“Nimefanya kazi ya boda boda sana pale Mariakani kwa sababu sikuwa na kazi nyengine. Changamoto ilikuwa kwenye visa wakati huo ambapo boda boda walikuwa wanaibiwa pikipiki zao wengine wanauawa.Ikafika wakati nikaanza kuchukia hii kazi ikanibidi niuze pikipiki zangu ili nianze masomo. Kwa sababu nilikuwa mtu wa kelele kelele, nikajua kabisa uanahabari utakuwa unanihusu,” amesema Robby Dallaz.
Baada ya kulipa karo ya shule, akajipata kwa rafiki yake Alphonce ambaye alikuwa akiishi kwake kwa muda akiwa shule hadi pale ambapo mke wa Alphonce alitaka kuja Mombasa eneo la Bakarani ili kuishi na bwanake. Kwasababu Robby Dallaz hakuwa na kazi ikizingatiwa kwamba alikuwa anatembea kutoka Bakarani hadi Katikati mwa jiji la Mombasa akienda shule akasaidiwa kujitoa kwa rafiki yake.
Kupitia nguvu ya marafiki, mwamba akajipata Likoni ambapo alisaidiwa na shilingi elfu mbili kuhamia nyumba ambapo atakuwa anaanza maisha akiwa kwake. Hayakuwa maisha rahisi kwake ila hakukata tamaa.
Historia ya Robby Dallaz ni ndefu ambayo imekuwa na changamoto mbali mbali lakini mbele kuna mwangaza kwani alianza kufanya kazi kama mwanafunzi katika kituo cha Televisheni cha K24 kama mpiga picha na ripota kisha sauti yake ikaanza kusikika kwa redio kupitia pilipili fm ndio baadae akajipata Radio Kaya na sasa Mo radio.
Upande mwengine, Robby pia alikuwa na ndoto ya kuwa msanii na alikuwa anafanya vyema japo pia alipitia changamoto zilizofanya aachane na muziki.
“Nilikuwa naimba tena nilikuwa niko na hitsongs nyingi sana, kila ngoma ilikuwa hit kule mtaani. Tulikuwa na kundi mimi na ndugu zangu lakini wakati huo studio zilikuwa kidogo.Nakumbuka nikimuomba msaada prodyuza Lai wakati huo kabla aokoke na akasema kama sina pesa ya kurekodi nisimsumbue kwasababu yuko kazini na studio ni ya kakake Jay Crack. Sikukata tamaa,Bangbelly ndio prodyuza maybe alitambua kipaji chake cha kuimba. Sema wakati huo akina Escober na wengine walikuwa wameshika sana,nakumbuka nikimuomba shabiki msaada wa kumisaidia kufikisha ngoma zangu kwa maredio akakataa kunisaidia lakiniu sina chuki naye kwasababu ilikuwa ni part of life tu,” Dallaz asema.
Kulingana na Robby Dallaz mbali na changamoto alizopitia kama msanii kuna mambo mengi ambayo anasema ameyashuhudia akiwa maneja ambayo yamefanya akatae kabisa mtoto wake wa kike kuja kuwa msanii.
“Siwezi tamani mtoto wangu wa kike aje msanii wa kuimba..No No No,” aliandika kupitia mtandao wake wa Facebook na kuongezea kwa akina P Diddy ni wengi hata hapa pwani.
Kulingana na maelezo yake kwenye The Hotseat, wasichana wanapitia wakati mgumu sana kwenye sanaa kwani amejionea mengi sana kwenye studio ambapo wasanii huenda ili walirekodi muziki.
Kuhusu kiki yake na Dogo Richie wa Kaya Records, Dallaz amesema haikuwa kiki kwani alikuwa anadaiana na yeye deni la kishkaji na pia alikuwa ameongea na Richy Ree kabla kuweka jambo hilo kwenye mitandao.Nia ya kufanya hivyo pia ilikuwa kuskuma ngoma mpya ya Dogo Richie aliyoifanya na Masauti na Trio Mio.
Maisha ya mahusiano ameyazungumzia pia kwamba hakuwa na uwezo wa kumuweka hadhgarani mpenzi wake kwani hakuwa amemlipa mahari na haikuwa rasmi ila kwa sasa kila kitu kipo wazi na rasmi na anampenda sana mpenzi wake ambaye pia ni mwanahabari, Caroline Mkamburi anayefanya na shirika la Mediamax.