Mombasa, Januari 31- Joto lazidi kupanda Ukanda wa Pwani huku kila msanii na mdau wa muziki akivutia kwake. Nembo ya ‘Ziki La Nazi’ imezua gumzo baada ya familia ya marehemu Ally B kudai kuwa haitakiwi kutumika tena, wakisema kuwa wao ndio wenye haki miliki ya nembo hiyo. Hii ni nembo ambayo imekuwa ikitumiwa na wasanii mbalimbali na kuonekana kama aina ya muziki wa Pwani.
Familia ya marehemu Ally B ilitangaza msimamo wake katika mahojiano na Mwanahabari Tizo wa Leo, hatua iliyozua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii. Kulingana na familia, yeyote anayetaka kutumia jina au nembo hiyo anapaswa kupata idhini yao kwanza.
Maswali yamezidi kuibuka mtandaoni, huku wengi wakijiuliza: Nani ndiye mmiliki halali wa nembo ya ‘Ziki La Nazi’?
Kwa mujibu wa maoni ya wadau na wasanii mbalimbali, akiwemo Steve Kipande maarufu kama Daddy Q, mwanzilishi wa nembo hiyo ni msanii Nguchi P, na si Ally B kama familia yake inavyodai. Kipande alieleza:
“Watu hawajui, jina ‘Ziki La Nazi’ lilianzishwa na Nguchi P (Mapipy) tulipokuwa kwenye mkutano wa wasanii wa Pwani miaka hiyo. Tulikuwa tunatafuta jina la jumla, na watu walipendekeza ‘Mombasani,’ lakini kwa kuwa kulikuwa na wasanii kutoka Kwale na Kilifi, Nguchi akapendekeza jina hili. Hata nembo yake ilichorwa na Shahidi George Uduny, maarufu kama Kingstin, pamoja na wasanii wengine.”
Steve Kipande aliendelea kwa kusema kuwa wengi hawajui historia ya muziki wa Pwani na wanaamini tasnia hiyo ilishajengeka, bila kuelewa juhudi zilizowekwa.
“Watu wengi hawajui sanaa ya Pwani. Wameamka kuona mifumo imewekwa, kisha wanaanza kudai wao ndio waanzilishi. Lakini sisi tumejenga, tukiwaangalia tu.”
Mtazamo huu pia umeungwa mkono na mtayarishaji wa muziki Tee Hits, ambaye alisisitiza kuwa ‘Ziki La Nazi’ si nembo ya Ally B, bali ni jina lililotumiwa kwa muda mrefu na wasanii wa Ukanda wa Pwani. Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Tee Hits aliandika:
“‘Ziki La Nazi’ haikuwa nembo au kauli mbiu ya mtu binafsi. Iliibuka baada ya mkutano wa wadau wa muziki na wasanii kutafuta jina litakaloakisi muziki wa Pwani, ndipo Nguchi P alipopendekeza jina hili. Tangu wakati huo, likawa likitumika.”
Tee Hits akaongeza:
“Nyimbo za Ally B, sawa, hatutaziimba, lakini ‘Ziki La Nazi’ nitatumia. Natoa wimbo mpya wiki ijayo uitwao ‘Ziki La Nazi.’”
Msimamo huu pia umeungwa mkono na msanii Susumila, ambaye alisema alitumia nembo hiyo hata kabla ya Ally B. Akizungumza kwa njia ya simu na Captain Nyota, Susumila alieleza kuwa alilitumia jina hilo katika wimbo wake na Timmy Tdat na pia kwenye kolabo aliyofanya na Avril, bila kuzua mzozo wowote.
Kwa hivyo, swali linabaki: Je, familia ya Ally B ina msingi wowote wa kudai umiliki wa nembo hiyo? Na je, Nguchi P atazungumziaje suala hili?